Viongozi wa Dini Wataka Kutungwa Sheria ya Bima ya Afya Kwa Wote
VIONGOZI wa dini wameiomba serikali kuharakisha mchakato wa Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ili ipatikane sheria itakayowazesha watu masikini kupata huduma ya afya bila kuathiriwa na hali zao za kiuchumi.
Wametoa ombi hilo kwa serikali Agosti 27, 2021 jijini Dar es Salaam huku wakisisitiza kuwa Bima ya Afya kwa wote inawezekana.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Fredrick Shoo alisema kuwa tafiti za kitaalam zilizofanywa zimeonesha kuwa asilimia 26.4 (sawa na takribani milioni 15) ya Watanzania ni masikini hivyo hawawezi kumudu gharama za bima ya afya.
Askofu Shoo amesema suluhisho la kuwa na bima kwa wote ni serikali kuharakisha mchakato wa kuandaa muswada ili ukapitishwe na Bunge kuwa sheria.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislam nchini (BAKWATA Sheikhe Hamis Mataka alisema baada ya utafiti kuonesha kuwa kundi kubwa la Watanzania wanashindwa kumudu gharama za matibabu kwa kukosa bima, viongozi wa dini wamependekaza kuwepo kwa bima ya afya kwa wote.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kardinali Rugambwa Sr Sara Deogratius amesema kuwa gharama za matibabu zipo juu hivyo kwa kuwa wengi hawana bima hufika hospitalini wakiwa wamechelewa na kufanya ugonjwa ambao ungetibiwa kwa haraka kuwa changamoto zaidi.
“Hii inatokana na kukosa bima…atasema ninaenda kesho ninaenda kesho na hatimaye anajikuta katika hali mbaya…wito wangu kwa serikali ni kuomba huu mchakato wa bima kwa wote uweze kupewa kipaumbele,” alisema Dk Sara.
Chanzo: Habari Leo