Viongozi wa dini wazungumza kushamiri kwa Biashara ya Ukahaba

2 years ago By Nyimbo Mpya 634
Are you a music lover looking for the latest track to add to your playlist? Look no further. Get ready for an unforgettable musical experience as we present a song by Viongozi wa dini wazungumza kushamiri kwa Biashara ya Ukahaba.

Viongozi wa dini wazungumza kushamiri kwa Biashara ya Ukahaba


Viongozi wa dini nchini wameitaka Serikali kuingilia kati suala la kuongezeka kwa madanguro katika jamii ili kupunguza maambukizi ya magonjwa, ikiwemo Covid-19.

Wito huo wa viongozi wa dini umekuja baada ya kubaini kushamiri kwa biashara ya ukahaba kwenye madanguro ambayo yapo katikati ya makazi ya watu.

Baadhi ya viongozi, akiwemo aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda waliwahi kujaribu kukomesha biashara hiyo kwa kuwakamata makahaba, hata hivyo, jitihada hizo hazikuzaa matunda.

Imebainika kuwa bado kuna madanguro mengi jijini Dar es Salaam, ambapo wanawake wenye umri kati ya miaka 14 – 40 wanajihusisha na ukahaba. Viongozi wa dini wamelaani biashara hiyo haramu na kutoa wito kwa Serikali, hasa zile za mitaa kutokomeza biashara hiyo katika makazi yao ili kuinusuru jamii dhidi ya maradhi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binaadamu kwa Jamii ya Viongozi wa Dini, Askofu Wiliam Mwamalanga anasema viongozi wa Serikali za Mitaa wapewe maelekezo ya kukabiliana na jambo hilo.

Anasema bado Serikali haijafanya jitihada za kutosha kukomesha biashara hiyo, ndiyo maana imeendelea kuwepo kila mwaka na jamii imeanza kuona ni jambo la kawaida.

“Serikali za mitaa zichukue hatua kukabiliana na madanguro kwa sababu yapo kwenye mitaa yao wanayoishi. “Nina uhakika viongozi hao wakifanya kazi yao ipasavyo, madanguro yote yatafungwa. Wenyeviti wa Serikali za Mitaa waelimishwe, wanaweza kabisa kuondoa tatizo hili,” anasema Askofu Mwamalanga.

Kiongozi huyo wa dini anasema amefuatilia suala hilo na kubaini kwamba sababu zinazowafanya wanawake kujiingiza kwenye biashara hiyo ni ugumu wa maisha unaotokana na ukosefu wa ajira.

Hata hivyo, anasema ukahaba siyo ajira ya staha kwa sababu licha ya kuhatarisha maisha yao, inawatenganisha na Mungu na pia jamii inayowazunguka.

“Hatari ninayoiona ni kwamba watoto wa shule za msingi na sekondari nao wamo kwenye madanguro hayo. Tunatengeneza jamii ya namna gani?

“Serikali kupitia wizara ya afya isilifumbie macho jambo hili, tena wakati huu tunapambana na ugonjwa wa corona, ni hatari zaidi. Wasipodhibitiwa watakuwa wanaeneza maambukizi kwa wengine,” anasema askofu huyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema biashara hiyo ni kitendo kiovu katika jamii kinachosababisha matatizo mengi, yakiwemo maradhi.

Anasema biashara hiyo haikubaliki katika jamii kwa sababu imekuwa chanzo cha matatizo mengi, ikiwemo kuongezeka kwa watoto wa mitaani pamoja na yatima.

“Serikali inapaswa kuchukua hatua, kwa sababu biashara hiyo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa maradhi, hasa Ukimwi, ongezeko la watoto wa mitaani na wanaoishi katika mazingira magumu,” anasema Sheikh Mataka.

Anabainisha kuwa wao kama viongozi wa dini wamekuwa wakijitahidi kutoa mafundisho, lakini vitendo hivyo vya uvunjifu wa maadili vimekuwa vikiendelea, jambo ambalo anasema ni dhambi na havikubaliki kwenye jamii.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima anasema ni kweli amri za Mungu zinavunjwa, lakini kama viongozi wa dini wanalo jukumu la kufundisha ili maadili yafuatwe.

“Kwa upande wangu siwezi kulizungumzia kwa kuwa sina takwimu wala ushahidi, niseme tu kwamba tunajua amri za Mungu zinavunjwa,” alisema Padri Kitima.

Mchungaji wa Kanisa la PCT lililopo Segerea, Didas Msonga anasema kuongezeka kwa vitendo vya ukahaba ni ishara ya hofu ya Mungu kupungua katika jamii, ndiyo maana wanaume na wanawake wanajihusisha na mambo ya ukahaba.

Anasema kwa kuwa ni jambo ambalo halikubaliki katika jamii, serikali ina wajibu wa kuchukua hatua ili kuwalinda wananchi wake, hasa wasichana wadogo wanaoingia kwenye ukahaba kwa sababu ya hali ngumu ya maisha katika familia zao. “Sisi kama viongozi wa dini tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuwataka waumini wamwabudu Mungu wao lakini serikali nayo iweke mikakati ya kukomesha madanguro huko mitaani,” anasema mchungaji huyo.

Mratibu wa huduma za makundi maalumu kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Danieli Sendoro anasema kushamiri kwa vitendo hivyo ni tatizo la mmomonyoko wa maadili na kukata tamaa kwa mabinti.

Anasema kwenye mambo ya maadili kuna vitu viwili ambavyo kundi moja linafanya vitendo hivyo kwa sababu wamechagua kama mfumo wa kuwawezesha kuishi na hii ni kutokana na wao kushindwa kudhibiti uendeshaji wa maisha kwa njia nyingine na kufanya vitendo vya ukahaba ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

“Kundi lingine ni mfadhaiko katika mabadiliko ya dunia, huletwa na kundi ambalo huhangaika kufanya maisha ili yawe kama wao wanavyotaka, ikiwemo kuuza miili yao na sio kwaajili ya kupata kipato, kwao imekuwa kama utamaduni,” anasema Mchungaji Sendoro.

Chanzo: Mwananchi

Download Now 634
Install Android App
Developer: Tanzania Tech Media
Price: Free
  • Nyimbo Mpya Screenshot
  • Nyimbo Mpya Screenshot
  • Nyimbo Mpya Screenshot
  • Nyimbo Mpya Screenshot
  • Nyimbo Mpya Screenshot