Serikali Yaagiza Askofu Gwajima Kukamatwa
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ameliagiza Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ( Takukuru) kumkamata na kumhoji mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima ili athibitishe kauli anazozitoa dhidi ya Serikali na viongozi kuhusu chanjo ya Uviko 19.
Dk Gwajima ametoa agizo hilo leo Jumanne Agosti 17, 2021 katika kijiji cha Kyatunge wilayani Butiama akibainisha kuwa Askofu Gwajima amekuwa akitoa taarifa za kupotosha kwa makusudi jambo linaloivuruga wizara yake na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kwa muda sasa Askofu Gwajima amekuwa akisisitiza kuwa hatakubali kupatiwa chanjo ya kukabiliana na Uviko-19 na kuwataka waumini wake kutojitokeza kwenda kuchanja.
Askofu Gwajima ametoa msimamo huo wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai akiwaasa wabunge kujitokeza kuchanja na kwamba japo ni hiyari lakini hakuna hiyari ya kuwaambukiza wengine Uviko-19.
Chanzo: Mwananchi