Nabii Afikishwa Kortini Madai ya Ubakaji
NABII Jackson Ibrahim (30), ambaye ni kiongozi mkuu wa Kanisa la The Power of Perfection Ministry, maarufu kama ‘nguvu ya utimilifu’ amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, akikabiliwa na kesi ya kumbaka mtoto wa miaka 15.
Kiongozi huyo wa dini, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda anayesikiliza shauri hilo. Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Blandina Msawa, alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 18, mwaka huu akiwa eneo la Majengo, jijini Arusha.
Nabii huyo anadaiwa kumbaka msichana huyo, huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha kifungu cha 130 (1) (2) (A) na (131) (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria iliyofanyiwa marejeo Mwaka 2019.
Baada ya kusomewa kosa linalomkabili, Nabii huyo alikana kutenda kosa hilo na Hakimu Kisinda, alisema dhamana dhidi ya mshtakiwa iko wazi. “Dhamana ya mshtakiwa iko wazi, unapaswa kuwa na wadhamini wawili,
ambao wana mali zisizohamishika zenye thamani ya Sh. milioni 10, kila mmoja.
“Pia, kuanzia sasa hupaswi kusafiri ama kutoka nje ya Mkoa wa Arusha, bila kuwa na kibali cha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.” Muda mfupi baada ya mshtakiwa kutimiza masharti hayo ya dhamana, Hakimu Kisinda, aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 13, mwaka huu litakapotajwa tena mahakamani humo.
Chanzo: IPP