Kenya: Maaskofu Wapiga Marufuku Siasa Madhabahuni
Viongozi wa dini kutoka Vihiga Kenya wameunga mkono hatua ya kanisa la Kianglikana kupiga marufuku viongozi kufanya siasa madhabahuni.
Wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Africa Divine Church (ADC) John Chabunga na Kanisa la Gospel Center, Askofu wa Mbale Isaac Wawire, viongozi hao wa dini walipiga marufuku wanasiasa kujihusisha na siasa mazishini. “Licha ya kwamba tunaalika kila mmoja kuhuddhuria hafla zetu, tunamuunga mkono Askofu Mkuu wa ACK Jackson Ole Sapit kwamba hatutatoa nafasi kwa wanasiasa kuleta mgawanyiko katika mikutano,” Wawire alisema. Alisema, hata hivyo, kanisa litatambua uwepo wa viongozi wote wa kisiasa, lakini hawatapewa fursa za kuhutubia waumini kuhusiana na sera zao za siasa.
Walitoa wito kwa viongozi kuhudhuria ibada kama waumini wengine wa kawaida. “Kama viongozi wa kanisa, tunachosema ni kwamba hatuwezi kukaa chini na kuchangia chuki katika makanisa yetu. Kwa hivyo, ikiwa wanasiasa wetu wataendelea na tabia hii basi hatutakuwa na budi ila kuwazuia kuzungumza katika makanisa na mazishi,” alisema Chabuga. Viongozi wa kidini wakati uo huo walimwuliza Rais Uhuru Kenyatta kusuluhisha tofauti zake na Naibu Rais William Ruto kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Walihisi kuwa mgawanyiko unaoendelea kati ya viongozi hao wawili wakuu unachangia chuki kati ya Wakenya. Mnamo Jumapili, Septemba 12, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana, Jackson Ole Sapit alipiga marufuku siasa wakati wa ibada ili kuzuia siasa kanisani. “Nimepiga marufuku wanasiasa kupewa nafasi ya kuzungumza katika makanisa yetu yote. Ninawashauri hata waandishi wa habari ambao hupanga vifaa vyao, wasijishughulishe kwa kuwa wanasiasa hawatazungumza hapa, labda baada ya ibada,” alisema Sapit.
Chanzo: TUKO