Malezi ya kipadre, kiutu na kijamii yaanzie kwenye familia

2 years ago By Nyimbo Mpya 1.1K
Are you a music lover looking for the latest track to add to your playlist? Look no further. Get ready for an unforgettable musical experience as we present a song by Malezi ya kipadre, kiutu na kijamii yaanzie kwenye familia.

Malezi ya kipadre, kiutu na kijamii yaanzie kwenye familia


Habari

Published on April 20, 2021

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, WAWATA, Dar Es Salaam.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, inayoadhimishwa tarehe 25 Aprili 2021, inanogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu anakazaia umuhimu wa ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Ni katika muktadha huu, Seminari ya Bikira Maria, Visiga, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumamosi tarehe 17 Aprili 2021, imeadhimisha mahafali ya tatu ya Kidato cha Sita, kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya waseminari wadogo 27, ambao kwa sasa wanajiandaa kwa mitihani na hatimaye, kutoa msimamo kuhusu wito wao. Itakumbukwa kwamba, mwaka 2020 waseminari 24 walihitimu kidato cha sita, kati yao 10 waliendelea na malezi ya Kipadre, saba kati yao, wakiwa ni kwa ajili ya Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Ni malezi yanayokita mizizi yake katika: Sala, Kazi, Nidhamu na Elimu!

Padre Henry Mchamungu, Jalimu wa Sheria za Kanisa toka Seminari Kuu ya Segerea ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa nia ya kuombea miito, ili wahitimu waweze kufanya maamuzi sahihi mintarafu wito huu Mtakatifu. Bikira Maria Msimamizi wa Seminari ya Visiga aendelee kuiombea Seminari hii, ili vijana waweze kupata malezi na makuzi bora kwa ajili ya wito na zawadi ya Upadre, tayari kuyatakatifuza malimwengu, hata kama wanafunzi wote hawa hawatafikia Daraja Takatifu ya Upadre. Walipende, walilinde na kulihudumia Kanisa la Kristo, ili mwisho wa safari yao hapa duniani waweze kufika mbinguni. Padre Henry Mchamungu amewatia shime waseminari hawa kupiga moyo konde na kusonga mbele katika malezi na majiundo ya Kipadre. Amewashukuru wazazi na walezi kwa malezi, makuzi yao pamoja na kuwawezesha kupata elimu Seminarini hapo. Katika hatua hii tete ya kuamua hatima ya maisha na wito wao, wazazi wametakiwa kuwachaguliwa watoto wao fungu lililobora zaidi, yaani Daraja ya Upadre, ikiwa kama watoto wao watapenda kupata ushauri kutoka kwa kwao na kamwe wasiwe ni vikwazo na watu wa kupindisha msimamo wa watoto wao!

Ifuatayo ni hotuba ya Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti Taifa, Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA aliyoitoa kwenye mahafali ya tatu ya Kidato cha Sita, Seminari ya Bikira Maria, Visiga, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Amekazia umuhimu wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani na seminari kama kitovu cha malezi na majiundo ya kitawa. Upendo ndani ya familia unogeshe malezi na makuzi ya watoto na kwamba, Mtakatifu Yosefu awe mfano bora wa kuigwa katika kutekeleza dhamana na majukumu ya maisha ya ndoa na familia pamoja na malezi kwa watoto wao. Mhashamu Baba Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Mheshimiwa Baba Gambera Philip Tairo, Mapadre, Masista, Mashemasi, Mafrateri, Wanafamilia wote wa Seminari ya Bikira Maria, Visiga, Kitalu cha Miito ya Kipadre, Viongozi wa Serikali, Wawakilishi wa WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam, kwa namna ya pekee Wahitimu wetu kidato cha sita na wadogo zao wanaobaki, wazazi wa wahitimu, wageni wote waalikwa Mabibi na Mabwana: “Nuru yetu iangaze, ili tukayatakatifuze malimwengu”.

Ndugu zangu wapendwa, tunatambua kwamba, waseminari hawa baada ya siku chache wataingia kipindi cha mpito kuendelea na hatua nyingine ya malezi au kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha yao kadiri ya mpango wa Mungu. Hiki ni kipindi muhimu sana katika maisha ya waseminari ambao sehemu kubwa ya maisha yao, ilijengeka katika msingi wa: sala, masomo na kazi kwa pamoja vikifungamanishwa na nidhamu, kwa kufuata na kuzingatia ratiba ya shule. Baada ya siku chache hawa watakuwa vijana huru kabisa wanarejea mitaani na huko watakutana na vijana wenzao kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania na dunia katika wengine wakiwa ni marafiki wa zamani: shule za awali, sekondari na majirani. Ni wakati wa kunafsisha zile tunu msingi za maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu katika kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii na hii itatasaidia kuonesha tofauti yao na waliosoma shule ambazo si seminari. Ni katika muktadha huu, napenda kujielekeza zaidi katika mambo matatu kwa kifupi kabisa: Mwongozo wa malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionalis Sacherdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”.

Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu kwa kukazia umuhimu wa malezi katika familia. Hatimaye, ni kuhusu maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia”. Mwongozo wa malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Unabainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, kuanzia kwenye familia kama Kanisa dogo la nyumbani, ili kweli wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia!

Sura ya Pili ya Mwongozo huu inapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre: Walezi na walelewa wanapaswa kuunganika na Kristo ili aweze: kuwaongoza, kuwachunga na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Dhamana ya Kanisa katika kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu. Mwongozo unasema, Seminari ndogo na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wadogo wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili. Ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili yanayoweza kufafanuliwa kuwa ni: Utii, Ufukara na usafi kamili au useja. Walezi wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo, hapa walezi ni kuanzia wazazi, mapadre na jumuiya nzima ya Seminari ya Bikira Maria, Visiga katika ujumla wake.

Ni matumaini ya Kanisa Jimbo kuu la Dar es Salaam kwamba, mambo haya msingi yamezingatiwa katika hatua zote za malezi na leo hii, waseminari wa kidato cha sita, wanaweza kufunga ukurasa huu, tayari kujiandaa kuingia kwenye nyumba ya malezi pale Kijichi, kwa wale wanaohisi kuwa bado wanajisikia kuwa na wito wa Upadre. Kwa wale ambao hawataendelea na wito huu kutokana na sababu mbalimbali basi wawe ni mabalozi wema na watakatifu huko wanakokwenda, ili kwa malezi na majiundo yao hapa Visiga Seminarini waweze kuwa kweli ni mwanga wa ulimwengu na chumvi ya dunia. Tunayo mifano ya viongozi wakuu katika sekta mbalimbali waliotamani kuwa Mapadre, lakini Mwenyezi Mungu akawaonesha wito wao. Kwa mfano ni Makamu wa Rais Dr. Philip Mpango, IGP. Simon Siro bila kumsahau Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Bila shaka hata miongoni mwa wazazi na walezi mlioko hapa kuna baadhi yetu walitamani kuwa Mapadre au watawa, lakini Mwenyezi Mungu ana makusudi kwa kila mmoja wetu.

Mtakatifu Yosefu ni Msimamizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Bila shaka mtakumbuka kwamba, Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa tarehe 8 Desemba 2020 na utahitimishwa tarehe 8 Desemba 2021. Waraka wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ni, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu”: Papa Francisko anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu kuwa ni “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana. Hizi ni sifa ambazo tunapaswa kuzimwilisha katika maisha, malezi na makuzi ya watoto wetu.

Kuna maendeleo makubwa ya sayansi ya mawasiliano ya jamii yanayojidhihirisha kwa namna ya pekee katika matumizi ya: luninga, internet pamoja na mitandao ya kijamii, yanayochangia kwa kiasi kikubwa katika kulea dhamiri za watoto wadogo na vijana. Matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii ni hatari sana katika kuunda dhamiri za watoto na vijana. Wazazi tujitahidi sana kuwa karibu na watoto wetu na hasa wale ambao wanatumia muda mrefu zaidi wakiwa nje ya familia kwa sababu ya masomo kama ilivyo kwa hawa wa Visiga. Tujitahidi kuwafahamu vyema marafiki wa watoto wetu, ili tuweze kuwasaidia kukua katika njia njema inayozingatia kanuni maadili na utu wema! Wazazi tuwe mstari wa mbele kuwarithisha watoto wetu tunu msingi za Kiinjili, Imani na Mafundisho makuu ya Kanisa. Na hapa niwasihi sana Watoto wangu, kila jambo lisilo na mipaka linaweza kuwa maangamizi ya ndoto yako. Mama mnoko, baba katili nuksi na majina yote mabaya mtatubatiza, lakini kesho yenu ni muhimu sana kwetu, kanisa na taifa na ndio maana tunapenda kuwa sehemu ya makuzi yenu.

Wazazi tukumbuke kusali na kuwaombea watoto wetu kwa Mwenyezi Mungu si tu wakati wa mitihani, bali uwe ni utamaduni wetu ili waweze kuwa ni watu wema; tuwafundishe pia kusali kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya utakatifu, haki, amani, upendo, msamaha na maridhiano. Seminari hii iko chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Nitakosa fadhila ya unyenyekevu nisipoitaja Familia Takatifu. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu waliochangia kwa kiasi kikubwa malezi na makuzi ya Mtoto Yesu, dhamana na wajibu unaopaswa kuendelezwa na kutekelezwa na wazazi hata katika ulimwengu mamboleo. Mtoto Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli, kumbe, alihitaji malezi ya kiutu katika ubinadamu wake – Baba na Mama walifanya kazi yao. Kumbe, wazazi na walezi tunapaswa kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya watoto wetu katika hatua mbalimbali, hasa wakiwa wangali wadogo, kwani waswahili husema, “Samaki mkunje angali mbichi, akikauka hakunjiki tena”. Wazazi na walezi wakiwekeza vyema kwa watoto wao hapana shaka kwamba, hata maisha yao huko mbeleni, yatakuwa ni ya heri na baraka tele!

Familia iwe ni kitovu cha msamaha wa kweli, kwa kutambua kwamba, kukosa na kukoseana ni sehemu ya udhaifu wa kibinadamu, kutubu, kusamehe na kupatana ni mwanzo wa mchakato wa utakatifu wa maisha. Wanafamilia wajifunze kusema: Naomba, Asante na Samahani; maneno yanayoweza kuisaidia familia kuishi kwa amani na utulivu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko kuhusu wito wa familia na maisha ya ndoa na familia. Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka mitano tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, siku Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2021, Mama Kanisa amezindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kumi ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Miaka mitano imegota tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”.

Kumbe, maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni muda muafaka wa kuanza kuvuna matunda yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano katika medani mbalimbali za maisha: kikanisa na kijamii. Ni nafasi ya kutafakari changamoto, fursa na matatizo yaliyopo na kuendelea kuzifanyia kazi. Changamoto ni kukubali na kuupokea Wosia ambao umesheheni maneno ya ujasiri, chachu ya mabadiliko pamoja na mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na watu wa Mungu. Familia zinahitaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, zitakazowawezesha wanandoa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia katika ujumla wake. Familia inapaswa kusimikwa katika upendo wenye huruma, kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, inayotangaza na kushuhudia uwepo mwanana wa Mwana wa Mungu. Katika shida na magumu, familia zisaidiwe kwa hali na mali, ili kuweza kupita vipindi hivi vigumu kwa kusindikizwa na upendo wenye huruma. Familia zinazoogelea kwenye shida na ugumu wa maisha zisikilizwe na zisaidiwe.

Mikakati mbalimbali ya shughuli za kichungaji iwasaidie wanandoa kupyaisha upendo wao kila kukicha. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kushirikishana sera, mikakati na shughuli za kichungaji. Lengo ni kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika maisha ya wanandoa. Umefika wakati wa kubadili fikra, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa familia kama kiini cha shughuli za kichuhngaji katika ngazi mbalimbali za maisha ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia ziwe ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kwa kuendelea kuwa ni Katekesi hai. Maisha yao yawe ni ujumbe wa matumaini hasa miongoni mwa vijana, ili hata wao waweze kutekeleza ndoto katika maisha yao. Huu ni muda muafaka wa kuwaunda na kuwafunda wadau wa sera na mikakati ya utume wa familia. Mkakati huu uanzwe kutekelezwa tangu mwanzo kabisa Mseminari anapoingia seminari kuu. Wanafamilia waoneshe neema inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa, ili waweze kujizatiti, tayari kupambana na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo.

Viongozi wa Kanisa wawe mstari wa mbele kuupokea na kuumwilisha Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” sanjari na kujifunza kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya familia. Waamini waendelee kumjifunza Mtakatifu Yosefu, kwa kujikita katika ukarimu, utii, nguvu na kuthamini kazi na ajira. Kanisa liendelee kuwa ni Mama na Mwalimu kwa familia; kwa kusikiliza familia kwa makini pamoja na kuendelea kujiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu.

Chanzo: www.vaticannews.va

Download Now 1.1K
Install Android App
Developer: Tanzania Tech Media
Price: Free
  • Nyimbo Mpya Screenshot
  • Nyimbo Mpya Screenshot
  • Nyimbo Mpya Screenshot
  • Nyimbo Mpya Screenshot
  • Nyimbo Mpya Screenshot