Kenya: Mwanaume Ambaye Hajawahi Kwenda Kanisani Wala Kwenye Mazishi Abatizwa
Katika miaka 92 ambayo Owuor Nyapoya kutoka Usenge katika kaunti ya Siaya ameishi, hajawahi kukanyaga kanisani wala kuhudhuria mazishi.
Ni kipindi ambacho mvuvi huyo amekuwa mtu tofauti sana duniani. Hata hivyo, hayo yote yalikuja yakabadilika wakati aliamua kwenda katika Kanisa Katoliki la St. Martin na kubatizwa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Sunday Standard, Nyapoya alikuwa amevalia shati nyeupe, rangi ya kijivu na viatu vyeusi. Kulingana na Padri Stephen Ouma, ambaye anasimamia Parokia hiyo, Nyapoya alikuwa mtu mzee zaidi kwake kuwahi kubatiza katika maisha yake yote kama mtumishi wa Mungu.
Nyapoya alisema kuwa aliamua kubadilisha maisha yake ya kiroho kwa sababu amekuwa na bahati ya kuishi maisha marefu kuliko watu wengi.
“Si watu wengi wa umri wangu walifaulu kuishi na Ukimwi kwa sababu ya maisha waliokuwa wanaishi. Kulikuwa na chakula kingi, pesa na wanawake,” alisema.
Alikumbuka siku za nyuma wakati alipuuza juhudi za familia yake kumshinikiza aokoke. Nyapoya alifichua kuwa hajawahi kwenda hospitalini na hakujiunga na shule kwa sababu baba yake hakuwa anathamini masomo. “Tulikuwa tunachunga mifugo ya baba yangu na wakati nilikuwa mtu mzima, niliamua kuwa mvuvi kwa sababu hiyo tu ndio ilikuwa shughuli ambayo watu wengi walikuwa wanafanya kuliko ukulima,” alisema.
Ubatizo ulifungua ukurasa mpya katika maisha ya Nyapoya, ambayo yataondoa machngu ambayo alisema yalikuwa yamemjaa moyoni. Padri Stephen Ouma alimbatiza Nyapoya kama Paul, na kufungua ukurasa mpya katika maisha yake ya Ukristo.
Padri huyo alisema alimpa jina jipya kulingana na maandiko ya Bibilia ambayo huashiria mabadiliko. “Paul alikuwa mtenda dhambi lakini aliona mwangaza na alibadilika. Mzee huyu alikubali na hivyo sikuwa na budi bali kumuandaa kwa ufalme wa Mungu,” alisema Padri Ouma.
Chanzo: TUKO