App ya YouVersion Bible Yasheherekea Kwa Kupakuliwa na Watu Milioni 500 Ulimwenguni
Wiki iliyopita App ya Biblia ya YouVersion yasherehekea hatua kubwa kwa kupakuliwa na watu milioni 500, na kuifanya kuwa app pekee ya ki-imani kuwahi kufikia hatua hiyo ulimwenguni.
Programu hiyo yenye umri wa miaka 13 ilizinduliwa mwaka wa 2008 kama moja ya app 200 tu za bure katika iOS App Store na kufanikiwa kuwa maarufu kwa haraka na kuwa app pekee ya Biblia iliyopakuliwa zaidi ulimwenguni.
Kwa mujibu wa toleo la habari kutoka Life.Church inasema mpaka kufikia mwaka 2021, Sura mbalimbali za Biblia zimesomwa au kusikilizwa zaidi ya mara bilioni 64, ambalo ni ongezeko la asilimia 21 ikilinganishwa na 2020 na asilimia 56 ikilinganishwa na 2019.
“Ingawa baadhi ya watu wanadai kuwa Biblia haina mashiko na ushiriki wa Maandiko kwa watu wengi unapungua, Lakini upakuaji wa app hii kwa watu milioni 500 umethibitisha vinginevyo,” alisema mwanzilishi wa YouVersion Bobby Gruenewald.
“Biblia inaendelea kuwa muhimu na ina uwezo wa kubadilisha maisha ya mtu. Ndio maana tunafurahi kusherehekea hatua hii muhimu. Sio tu kwa sababu ya idadi kubwa watu waliopakua app hii, lakini ni kwa sababu kila aliyepakua app hii inawakilisha nafasi kamili ya mtu kuingia ndani zaidi katika imani yake na kuwa karibu na Mungu.”
“Katika miaka kadhaa iliyopita, tumemwona Mungu mara kwa mara akifanya zaidi ya vile tunavyoweza kufikiria kupitia YouVersion,” Gruenewald alisema.
“Kwa vile app hii imekua kwa kasi kufikia watu katika kila nchi duniani na kubadilisha mamilioni ya maisha ya watu, imani yetu pia imeongezeka katika kuzitazama fursa mpya. Tunaamini huu ni mwanzo tu kwa YouVersion. Tuna maono mapya ya wapi Bible App inapoelekea, na tunayofuraha kuzindua vipengele vipya kwa mwaka wa 2022 ili kuwahudumia vyema wachungaji na viongozi wa makanisa.” alimalizia