Aina tano (5) za Watumishi

1 year ago 1357
Aina tano (5) za Watumishi. Get ready for an unforgettable musical experience as we present new song by Aina tano (5) za Watumishi Stream and download below.

Aina tano (5) za Watumishi Song


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote. Karibu tujifunze Neno la MUNGU la maarifa sahihi ya kutusaidia kujua na kutambua ili tubaki katika kusudi la MUNGU.

Natamani kila mtu atakayeliona somo hili popote alisoma lote hadi mwisho.

Leo nazungumzia aina tano za watumishi, somo langu sijaliita aina tano za watumishi wa MUNGU kwa sababu baadhi yao sio watumishi wa MUNGU bali watumishi wa mashetani, ndio maana nimeita tu aina 5 za watumishi maana baadhi yao ni watumishi wa MUNGU na wengine sio.

Wakati mwingine nimewahi kuulizwa namna ya kumtambua mtumishi wa kweli na nilitoa majibu vile ROHO wa MUNGU alivyonijaalia lakini hapa nataka nikutajie aina hizo za watumishi na utamtambua nani ni nani ambaye huwa unamuona akitumika.

Aina hizi tano zinahusisha Wachungaji wote, Maaskofu wote, Mitume wote, Wainjilisti wote, Waalimu wote, Manabii wote, Waimbaji wote, Wahubiri wote, Wafundishaji wote na kila anayemtumikia katika mambo ya kiroho kwa karama mbalimbali na huduma mbalimbali, kila mmoja katika hao anaangukia katika kundi mojawapo kati ya haya matano.

Jambo la kujua ni kwamba hizi ni siku za mwisho na watumishi wa kila aina watakuwepo, wakweli watakuwepo, waongo watakuwepo, wasanii wa kihuduma watakuwepo na waigizaji wa kihuduma watakuwepo na mawakala wa shetani wengi watakuwepo, ndio maana Biblia inatutaka sisi tulio Kanisa kumchunguza kila mtu na huduma yake au mafundisho yake kama mtu huyo anatokana na MUNGU au anatokana na maashetani.

1 Yohana 4:1 ”Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.”

Kanisa la MUNGU lazima liwe makini sana maana Bwana YESU pia anasema ” Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. -Ufunuo 3:11”

●Hivyo usipong’ang’ania wokovu halisi wa KRISTO YESU ujue anaweza kutokea Mtumishi wakala wa shetani akakuondolea taji yako ya uzima wa milele kwa yeye kukufundisha uongo ili uufuate na kukosa uzima wa milele.

●Wako pia watumishi ni wasanii tu hivyo wanaweza kumpoteza yeyote na akakosa taji yake ya uzima wa milele.

●Wako pia watumishi ni waigizaji yaani wanafanya utumishi kwa kuigiza na hivyo kuwapoteza watu.

●Wako pia watumishi ni matapeli tu na wengine wengi ni watumishi walio mawakala wa shetani.

Baada ya utangulizi huo sasa ngoja nikujulishe makundi 5 ya watumishi.

1. Mbwa mwitu

Matendo 20:29-30 ” Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.”

Hili ni kundi mojawapo la watumishi linalofanya kazi leo ulimwenguni.

Kwa kifupi hawa ni mawakala wa shetani waliojiingiza kwa siri katika Kanisa.

Hawa wameingia mikataba na shetani ili kuongeza watu wa kwenda jehanamu.

Ukisoma maandiko hapo juu tu unagundua kwamba watumishi aina ya mbwa mwitu kazi zao ni pamoja na

●kufundisha mapotovu yaani kuwapoteza watu kwa kuwatoa katika Wokovu wa KRISTO.

Baadhi ya watumishi walio mbwa mwitu walianzisha dini mbalimbali duniani na madhehebu ili kupinga Wokovu wa KRISTO YESU.

●Mafundisho yao ni ya kuwavuta watu kwao na sio kwa YESU KRISTO.

●Watawafanya baadhi ya watu wajiepushe na kweli ya MUNGU ambayo ni KRISTO YESU.

2 Timotheo 4:3-4 ” Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.

●Hawa kwa jina lingine ni mawakala wa shetani au maajenti wa kuzimu, wana ajenda ya kuhakikisha watu hawaendi uzima wa milele.

●Wanajichanganya na kondoo ili kuwala hao kondoo, yaani kuwafanya watu kuwa waabudu shetani.

●Wanafundisha mafundisho ya mashetani na kuwafanya watu wengi kumfuata shetani na sio kumfuata YESU KRISTO.

1 Timotheo 4:1-2 ”Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; ”

2. Mtu wa mshahara.

Yohana 10:12-13 ” Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.”

●Hili ni kundi lingine la watumishi, hawa wanaweza kuwa ni watumishi wa kweli wa MUNGU lakini hawafai kwa sababu hawawezi kufanya huduma bila kulipwa.

Wanaweza pia kuwa ni watumishi wa shetani na sio wa MUNGU.

●Mtu wa kundi hili kumjua ni rahisi sana maana ili akuombee umpe kwanza pesa, wana mbinu nyingi sana ila mbinu zote ni mbinu za kusaka pesa.

Mara anaweza kukuambia ”Toa milioni moja ili kujiunganisha na madhabahu yangu”

●Wamejaa mafunuo ya uongo yenye lengo moja tu kwamba pesa itoke.

●Wana sadaka ambazo Biblia haiagizi, unaweza ukasikia kwamba kuna sadaka ya kumuona Nabii yaani karani wa Kanisa anapokupanga kwenye foleni ya kumuona mtumishi anakuambia kwanza toa sadaka ya kumuona mtumishi huyo.

Watumishi wa namna hii huwatenga watu kimakundi kutokana na hali zao kiuchumi, unaweza ukasikia ”Watu 50 wenye laki tano kila mmoja wasimamame pale ili niwatabirie”

●Watumishi wa kundi hili ni watu wenye lengo la kujitajirisha tu.

●Mtumishi wa kundi hili anaweza hata akalikimbia Kanisa kama fungu la kumi ni kidogo kuliko alivyotarajia.

●Mtumishi wa kundi hili mambo ya kondoo sio ya kwake ila yeye analenga tu pesa.

●Hawa wanaweza kuingia katika huduma sio kwa wito kutoka kwa MUNGU bali ili wao watajirike.

Wanaweza kuingia kwenye huduma sio ili watu waokoke bali ni wao hao watumishi wawe matajiri.

●Hawa hata kwenye mafundisho yao ni nadra sana kuwasikia wanahubiri utakatifu au kukemea dhambi.

Wengi wao ni zao la vitu ambavyo vimejaa wakati huu viitwavyo maji ya baraka, mafuta ya upako, chumvi za upako, vitambaa vya upako, barafu za upako, keki za upako n.k

●Hawa Kanuni yao ni pesa kwanza.

Ndugu, ni kweli kabisa sadaka, zaka na dhabihu vina nguvu sana na ni vya muhimu sana katika Kanisa la MUNGU na huleta matokeo makubwa sana kwa mtoaji, lakini ni kama tu mtu huyo anatoa sio kwa shinikizo wala kudanganywa au kulazimishwa.

Mtu ambaye utoaji wake humletea matokeo makubwa ni yule anayetoa kwa moyo wa kumpenda MUNGU na hiari, tena akiishi maisha matakatifu.

Kutoka 25:1-3 ” BWANA akanena na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, na fedha, na shaba, ”

Ni kweli maandiko hapo juu yanaonyesha kwamba watu wa MUNGU inawapasa kila wakati kumtolea MUNGU matoleo lakini MUNGU halazimishi kutoa japokuwa kutoa ni kanuni muhimu ya kiroho.

Ni kweli kabisa MUNGU anataka tumtoleee matoleo safi na ya thamani na sio tu zile ziada kwetu lakini usitoe kwa kudanganywa na mtumishi ambaye sio Mtumishi wa MUNGU bali yeye ni mtu wa mshahara tu.

Kama ni mwimbaji basi bila pesa hafanyi huduma hata kama ni Kanisani kwao, kama ni mtaalamu wa vyombo basi ili afanye huduma kwanza alipwe.

Yaani yeye bila pesa hawezi kamwe kumtumikia MUNGU.

Watu wengi hutoa pesa baada ya vitisho kutoka kwa watumishi wasaka pesa, hiyo ni hatari sana.

Watumishi aina hii wana sifa nyingi, baadhi ni hizi kama zinavyosemwa katika Yohana 10:12-13

■Ni watu wa mshahara, bila mshahara hawafanyi huduma.

■Wao sio Wachungaji bali huchukua kondoo kutoka kwa wachungaji halisi.

Ni rahisi sana kumuona mtu ameanzisha Kanisa na baada ya muda ana washirika elfu kumi lakini wote walihamia pale wakiwa wameokoka ila walihama makanisa tu, kwa kanuni za ufalme wa MUNGU mtumishi huyo hata kama ana waumini sana elfu kumi lakini hajaleta faida kwenye ufalme wa MUNGU maana hajamfanya mtu hata mmoja kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi na kuacha dhambi, bali mtumishi huyo amepata waumini ambao tayari wameshaokoka ila kwa tamaa za maisha wamekimbilia pale ili labda wapate miujiza na miujiza hakuna ila usanii.

■Wao hawatengenezi kondoo bali huchukua kondoo kondoo kwenye mazizi ya wachungaji wengine.

■Wasipolipwa vizuri wanaweza kuikimbia huduma au kulikimbia kundi ili mbwa mwitu(mawakala wa shetani) wachukue nafasi

■Hawajali kondoo bali wao hujali pesa kutoka kwa kondoo.

Ninaposema haya sina maana kwamba watu wa MUNGU wasiwahudumie Wachungaji wao bali wawahudumie wachungaji wao na kuwajali sana lakini isitumike hila ili watu hao watoe pesa bali ni mtu mwenyewe moyoni mwake awiwe kutoa.

Au mtu awiwe kutoa baada ya kulisikia neno la kweli la MUNGU.

Sadaka zina nguvu sana katika ulimwengu wa roho lakini ziwe ni sadaka zinazotolewa kwa imani na kwa moyo wa upendo.

Watu wengi hutoa sadaka sio kwa imani bali kwa sheria na kulazimishwa au kushawishiwa na wachumia tumbo, hiyo ni hatari sana. Toa kwa MUNGU kwa msukumo wa ndani yako na sio kwa kushawishiwa.

Zaburi 96:7-9 ” Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake.”

3. Watumishi walio vuguvugu.

Ufunuo 3:15-16 ” Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. ”

Hili ni kundi lingine la watumishi na inawezekana kabisa kuna mtumishi anasoma hapa yeye yuko katika makundi zaidi ya moja ya watumishi.

Watumishi wa aina hii kwa YESU wapo na kwa shetani wapo.

■Wanaweza wakafundisha kweli ya MUNGU jana lakini baadae wanaingiwa na tamaa na kuanza kudanganya watu ili wajipatie sifa au pesa.

■Wanaweza kuchanganya uongo na ukweli ili tu wajaze Kanisa.

■Ni watumishi ambao hawana uhakika wa mambo mengi ya MUNGU.

■Watumishi wa aina hii wakati mwingine wamejikuta wanaingia urafiki na mbwa mwitu hivyo kujikuta wameacha Wokovu wa KRISTO na kuanza kuhubiri mambo yaliyo kinyume na kusudi la MUNGU la Wokovu.

Inawezekana kabisa robo tatu ya waumini wa Kanisani kwake ni walevi hivyo anaweza kuacha kuhubiri akikataza kunywa pombe ili tu asikimbiwe na waumini.

Kama mwanzo alikataza wanawake kuvaa suruali ibadani baadae unaweza ukashangaa kumuona akiruhusu wanawake kuvaa suruali, kumbe ni ili asikimbiwe na waumini.

Yaani unashangaa mtumishi jumapili moja alifundisha kwamba ni marufuku mwanamke kuvaa suruali Kanisani lakini wiki mbili baadae unamsikia tena akisema ”Kwa sababu ya utandawazi basi mnaruhusiwa wanawake kuvaa suruali na vimini kidogo” yaani kwa sababu yeye ni Mtumishi vuguvugu basi amekubali Biblia ibadilishwe na utandawazi kumbe ni ili asikimbiwe na waumini.

Baadhi ya sifa zao ni hizi.

■Huchanganya ukweli na uongo katika mafundisho yao.

■Huwachanganya kondoo na hivyo kuwaacha kondoo hawajui nini wafanye au nini wafuate.

■Hubadilika kwa sababu ya tamaa au mazingira.

■Wanaweza wakashindwa kukemea dhambi kwa sababu tu siku hiyo ibadani wamekuja matajiri au wanasiasa.

■Wengi ni watumishi watenda dhambi hivyo huacha kukemea dhambi hizo ambazo na wao huzitenda.

Mfano kama mtumishi ni mzinzi au mwizi ni ngumu kumuona akisema kwamba wazinzi na waasherati wataenda jehanamu kama Biblia inavyosema, maana hata yeye mwenyewe atakuwa anajisema

4. Watumishi wanaotembea kwenye maono ya wengine.

Matendo 19:11-16 ”MUNGU akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka. Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana YESU juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa YESU, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, YESU namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.”

Kundi hili la watumishi nalo limejaa sana.

■Sifa zao ni kuiga kama hawa wana wa Skewa walivyomuiga mtumishi Paulo, Watumishi wengi hata leo huiga na mengine huiga hata hawajui kama waliyemuiga ni wakala wa shetani au ni mtumishi mwaminifu wa YESU KRISTO.

■Watumishi wa kundi hili wanaweza kuwa hata hawajaokoka lakini kwa kuiga wanamtumikia MUNGU.

■Wanaweza kuwa wameokoka lakini wanatembea kwenye maono ya wengine.

■Hawa kazi yao kubwa ni kuiga na huiga hata yasiyowapasa.

Mfano unaweza kukuta mwanzilishi wa dhehebu lao alikuwa nabii na utashangaa wachungaji wote kutokea dhehebu hilo wanajiita ”nabii” hata kama kihuduma wao ni walimu au wainjilisti.

Watumishi wa kundi hili anaweza kumuona mtumishi anasema ”fireeeeeeeeeee” na watu wanaanguka basi na yeye tangu siku hiyo akiwa tu anaombea watu anachosema ni ”Fireeeeee” hata kama hajui aliyeanzisha hiyo ”Fireee” alikuwa na maana gani na katumwa na nani.

Unaweza ukamsikia mtu kazi yake ni kusema tu ”deeper deeper” kwa sababu tu ameiga kwa mtumishi maarufu fulani.

■Ndio maana kwa sababu ya kuiga yasiyo wapasa unaweza kumkuta Mtumishi anaombea watu 20 na hadi anamaliza mtu wa 20 kumuombea hutamsikia akisema ”Kwa jina la YESU KRISTO” Kwa sababu anatembea kwenye maono ya wengine ambao husema vimaneno fulani na watu wanaanguka.

Ndugu, kama ni wewe nakuombea kwa MUNGU Baba upate ufahamu wa kibiblia na sio kutembea kwenye maono ya wengine na ni maono ya uongo mengine.

■Kwa sasa baadhi ya makanisa hakuna tena kuomba kupitia jina la YESU KRISTO bali wao kwa sababu ya kutembea kwenye maono ya wengine basi kazi yao ni kutamka tu maneno fulani kwa sababu walimuona mtu mwingine anayatamka, wengine wakiona mtu anayedanganya watu kwa chumvi za upako au maji ya upako au mafuta ya upako na wao wanaanzisha.

■Mwingine anapoona wengine wanatumia leso za upako basi na yeye anaanzisha barafu za upako na kuwadanganya watu kwamba barafu zile zinapoyeyuka na matatizo yao yanayeyuka kumbe ni uongo maana barafu kwenye joto lazima tu iyeyuke hata kama kaishika mtumishi, yaani unaweza kukuta waumini muda wote wa ibada wameshika barafu bila kuomba na yule ambaye barafu yake inayeyuka wengine wanaambiwa wampigie makofu maana laana zake zimeyeyuka na kumbe ni uongo, na barafu hizo wameuziwa elfu 50 kila moja yaani ni utapeli uliobebwa na uongo.

Ndugu, usitembee kwenye utumishi wa kuiga, baki kwenye msingi wa Biblia.

Naipenda Biblia maana inatuagiza tuombe, na sio tu tuombe bali tuombe kupitia jina la YESU KRISTO.

Yohana 14:14 ” Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.”

Mfano hai ni huu kwa kuomba kupitia jina la YESU KRISTO kama Biblia inavyoagiza.

Matendo 3:6-10 ” Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la YESU KRISTO wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu MUNGU. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu MUNGU. Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango Mzuri wa hekalu; wakajaa ushangao wakastaajabia mambo yale yaliyompata.”

■Watumishi wa kundi hili husema waanzilishi wa madhehebu yao ndio kila kitu, kumbe ni uongo maana YESU KRISTO na Neno lake ndio kila kitu na sio wanadamu.

Kwa kuiga watumishi wa kundi hili unaweza ukamsikia anasema ”Nakuombea kwa Mungu wa baba yangu(Anamtaja)” hayo ni makosa makubwa sana maana Biblia inasema tuombe kupitia jina la YESU KRISTO na sio wanadamu.

■Watumishi wa kundi hili hujikuta miongozo yao na imani yote inategemea tu vitabu vya waanzilishi wa madhehebu yao, na sio Biblia takatifu, hiyo ni hatari sana.

5. Watumishi wa MUNGU wanaompenda MUNGU na wameitwa kwa kusudi lake.

Warumi 8:28 ” Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote MUNGU hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. ”

Hawa ndio watumishi pekee wanaofaa na wanastahili.

■Hawa wameokolewa na YESU KRISTO na wanamtumikia MUNGU kwa usahihi na utakatifu.

Nikitaka kuwaelezea hawa kwa kina basi inaweza ikanichukua masomo hata matano lakini kwa ufupi sana baadhi ya sifa zao zinapatikana katika Waefeso 4:11-15 kwamba ” Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa KRISTO ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa KRISTO; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KRISTO. ”

■Huwafanya watu wawe watakatifu kwa MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.

■Huujenga mwili wa KRISTO yaani huwafanya watu waokoke na kuwa wengi kwa YESU KRISTO huku wakimtii MUNGU na Neno lake.

■Huwafanya watu wakue kiroho kupitia fundisho la KRISTO.

■Huzipinga njia za udanganyifu.

■Hulitahadhalisha Kanisa juu ya hila za shetani na mawakala zake.

■ Huhubiri Neno sahihi la MUNGU wakati wote, wanakemea na kuonya inapobidi.

2 Timotheo 4:2 ”2 lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.”

■Wanamtii ROHO MTAKATIFU na huongozwa na yeye.

Warumi 8:14 ” Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. ”

■Mafundisho yao yanalenga watu waokolewe na YESU KRISTO(Luka 19:10, Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. ) na wafunguliwe vifungo na Bwana YESU(1 Yohana 3:8B,Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. )

Ndugu, naamini umejifunza na kulielewa vizuri Neno la MUNGU aliye hai.

●Sasa Je, wewe ni Mtumishi wa kundi lipi?

●Je wewe ni mhubiri wa kundi lipi?

●Je wewe ni Mwimbaji wa kundi lipi?

●Je Wewe ni Mchungaji, Mtume, Mwinjilisti, Nabii au Mwalimu wa kundi lipi?

●Je Mchungaji wako ni mtumishi kutokea kundi lipi?

●Je Huyo Mtumishi unayeshirikiana naye yuko kundi lipi na lipi?
“Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. – Ufunuo 2:11”
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Peter Mabula +255714252292
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Download Now 1357